Monday, May 3, 2010

Watano wafa ajalini wakitoka Mei Mosi

Watu sita, wakiwemo wafanyakazi watano wa Hazina Ndogo Shinyanga, wamefariki dunia katika ajali.

Habari kutoka eneo la tukio zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Daud Siasi zimeeleza kuwa ajali hiyo ilitokea majira ya saa 12 jioni katika Kijiji cha Buchambi wilayani Kishapu katika Barabara ya Shinyanga-Mwanza.

Kamanda Siasi aliwataja waliofariki kuwa ni pamoja na Mhakiki Mali wa Serikali mkoani Shinyanga, Mayombo Zedi (55), Ibrahimu Kibengele (59) mfanyakazi wa Bohari Kuu ya Mkoa, Charles Kasile (58), Juma Handule (45) dereva wa gari hilo.

Mwingine ni mfanyakazi wa Hazina Ndogo ambaye pia alikuwa maarufu kwa jina la Njoroge pamoja na Ngoyongo aliyetambulika kwa jina moja pia akiwa mfanyakazi wa Hazina Ndogo Shinyanga.

Alisema kuwa watumishi hao wa serikali wakiwa na gari aina la Land Rover 110 wakitokea wilayani Maswa kwenye maadhimisho ya sherehe za Sikukuu ya Wafanyakazi, Mei Mosi walipata ajali baada ya gari hilo kupinduka.

Katika ajali hiyo, mtu mmoja, Deusdedit Messu (56) alijeruhiwa na hali yake imeelezwa kuwa mbaya kutokana na kuumia kichwani, begani pamoja na sehemu nyingine za mwili.

Akielezea ajali hiyo, shuhuda Shija Mwandu alisema imetokana na mwendo kasi na kwamba gari hilo liliwa likifukuzana na jingine la Mamlaka ya Majisafi ya Mji wa Shinyanga na Kahama ambalo lilikuwa na bango la Mei Mosi.

“Wakiwa katika mwendo, gari hilo la mbele (la Majisafi) liliangusha bango, sasa hili gari la nyuma lilikuwa kasi, dereva wake akalikwepa ili asiligonge hapo ndipo gari lao lilipoanguka na kupinduka,” alisema Mwandu.

No comments:

Post a Comment