Monday, May 3, 2010

upepo mkali wakikumba kisiwa cha mafia

Upepo mkali umekikumba kisiwa cha Mafia na kuezua nyumba 53 na kusababisha maafa kwa wakazi wa Kaya 135 kukosa Makazi na wengine 7 kujeruhiwa vibaya.

Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Manzie Mangochie alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo lililopelekea maafa kwa Kaya 135.

Mangochie alisema kuwa, upepo mkali uliotokea upande wa Kusini kuelekea Magharibi ndio uliosababisha maafa hayo kwa kuezua mabati ya nyumba takribani 53 pamoja na kuharibu mazao kadhaa ikiwemo minazi.

Baada ya kutokea tukio hilo , Mangochie alisema kuwa, ofisi yake iliweza kutoa magari kadhaa ikiwemo ya kubebea wagonjwa na malori ya kuwahamisha kwa muda wahanga waliokumbwa na upepo huo.

“Baada ya kutokea kwa tukio hilo, sote tulifika eneo la tukio na kutoa msaada, kwa kweli lilikuwa la aina yake, napenda kuwatoa hofu wakazi waliokumbwa kuwa, kile sio Kimbunga kama walivyodhani, bali ni upepo mkali “Cyclone” hivyo wasiohofu chochote kwani Mamlaka ya hali ya hewa wataendelea kutoa taarifa zaidi juu ya hilo" alisema Mangochie.

Mangochie aliyataja maaeneo yaliyokumbwa na Upepo huo kuwa; Kilungeni A, Vunjanazi na Ismailia , ambapo kati ya nyumba hizo 53, Nyumba 50 zilikuwa ni makazi ya watu, mbili zilikuwa ni ofisi wakati moja ni gereji.


Majeruhi waliokumbwa ni pamoja na wanafunzi wanne wa shule ya msingi Kilimahewa Wasichana, walikimbizwa Hospitali na hali zao zinaendelea vizuri na wengine wawili walipatwa mshtuko wakati mmoja alivunjika mguu baada ya kuangukiwa na tofali.

No comments:

Post a Comment