Friday, August 24, 2012

Kumekucha bandari


Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amemsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Ephraim Mgawe, wasaidizi wake wawili na Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Cassian Ng'amilo kupisha uchunguzi wa wizi wa vitu mbalimbali yakiwamo makontena 40 ya vitenge, katika Bandari ya Dar es Salaam.

Dk Mwakyembe alitangaza uamuzi wake huo jana jijini Dar es Salaam, akiendeleza kile alichokifanya Juni 5 mwaka huu alipomtimua kazi aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Paul Chizi.
Hata hivyo waziri Mwakyembe hakutaja majina ya vigogo waliosimamishwa na badala yake alitaja nafasi walizokuwa wakizishikilia ambazo ni pamoja na Meneja wa Kituo cha Mafuta ya Ndege Kurasini (Kurasini Oil Jet - KOJ), Meneja wa Kituo cha Mafuta JET na mhandisi wa mafuta wa kituo hicho, baada ya kubainika kuwapo kwa wizi wa mafuta.

Kutokana na uamuzi huo, Dk Mwakyembe amemteua Mkurugenzi wa Usalama na Mazingira katika Wizara ya Ujenzi, Injinia Madeni Kipande kukaimu nafasi ya Mgawe.
Uamuzi huo umekuja baada ya kuwapo kwa taarifa za kupotea kwa makontena takriban 40 ya vitenge na vitu mbalimbali, yaliyokuwa yakipelekwa nchi jirani.

Dk Mwakyembe alisema ameunda kamati ya watu saba ambao hakuwataja majina ili kuchunguza wizi huo na kwamba amewapa wiki mbili tu, wawe wamekamilisha kazi hiyo.

“Nimeunda kamati ya kuchunguza suala hili, nimewapa hadidu za rejea zenye maswali 50..., majina ya waliopo katika kamati hii siyatangazi kwa sasa kwa sababu zangu binafsi,” alisema Dk Mwakyembe.

Alisema amechukua uamuzi huo baada ya kukutana na Bodi ya Wakurugenzi ya TPA juzi na kwamba hawezi kuvumilia kuona nchi inakosa mapato kwa sababu ya wizi uliokithiri.

Alisema kwa muda mrefu katika bandari hiyo ya Dar es Salaam, kumekuwa na malalamiko ya wizi wa vitu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ule wa vifaa vya magari, mafuta na kukithiri rushwa.

Alifafanua kwamba wizi huo umesababisha Bandari ya Dar es Salaam kukimbiwa na wateja ambao hivi sasa wanatumia bandari za Kenya, Msumbiji na Afrika Kusini.

“Makontena yanaibwa kama njugu, hivi sasa watu wa Rwanda, Uganda DRC hawaitumii tena Bandari ya Dar es Salaam, wanaona bora waingie hasara na wameanza kupitisha mizigo yao katika Bandari ya Mombasa Kenya, Beira nchini Msumbiji na Durban Afrika Kusini,” alisema Dk Mwakyembe.

Dk Mwakyembe alisema kuwa hivi karibuni mfanyabiashara mmoja mwanamke alitishia kuhamia nyumbani kwake, baada ya kuibiwa kontena zima la vitenge vilivyokuwa na thamani ya dola 180,000 za Marekani.

“Ni mambo ya ajabu sana hatuwezi kuwa na maendeleo kwa masuala ya ‘kisanii’ kama haya, nimeamua hivi kutokana na mamlaka niliyonayo na uamuzi nitakaouchukua najua wenzangu watanielewa,” alisema.

Wakati akieleza majukumu ya Mamlaka hiyo alisema, “Nimewataka TPA watambue majukumu yao jinsi yalivyo nyeti, nimewaeleza wazi kuwa imani ya wananchi imepungua sana kwa mamlaka hiyo.

“Kama waziri mwenye dhamana sitakuwa tayari kuona jambo hili linaendelea, hili suala haliwezi kuachwa likaendelea ni lazima uchunguzi ufanyike.”

Dk Mwakyembe alisema kuwa ameiagiza bodi ya wakurugenzi, kitengo cha sheria TPA kiuchambue upya mkataba wa Kampuni ya Kupakia na Kupakua Makontena katika Bandari ya Dar es Salaam (Ticts) na kumpatia taarifa Jumatano ijayo.

“Kontena likiwa na vitenge hata ukiweka askari 40 linaondoka, tumepoteza wateja wengi na watu wanaona bora kukimbilia bandari nyingine, nimewaagiza wauchambue upya mkataba huu,” alisema Dk Mwakyembe.

No comments:

Post a Comment